0
MKUU WA MKOA WA RUVUMA SAID MWAMBUNGU
Na Gideon Mwakanosya ,Songea.

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu amewataka wadau wa afya wa mkoani humo kuona umuhimu wa kuwekeza kwenye mfuko wa bima ya afya (NHIF) ambao tangu ulipoanzishwa umekuwa ukitoa huduma ya afya kwa jamiikwa gharama nafuu tofauti na ilivyokuwa awali.

Hayo aliyasema hivi karibuni kwenye semina ya utoaji mikopo ya vifaa tiba ,ukarabati wa majengo na dawa kwa vituo vya kutolea huduma za matibabu iliyofanyika kwenye ukumbi  wa mikutano wa hospitali ya serikali ya Mkoa (HOMSO) Manispaa ya Songea.

Alisema kuwa kazi nzuri ya Bima ya Afya imekuwa ikionekana hivyo  kila mdau wa sekta ya afya aone umuhimu wa kuchukuwa hatua ya kuwekeza kwa lengo la kuboresha huduma hiyo ambayo imekuwa iktolewa katika halmashauri mbali mbali mkoani Ruvuma.

Mwambungu alisema kuwa amewaagiza wakurugenzi wote wa halmashauri  na manispaa pamoja na wakuu wa Wilaya na wafanyabiashara kuanza mara moja kufanya mazungumzo ya kina na mfuko wa bima ya afya ili huduma ya afya iweze kutolewa zaidi.

Hata hivyo mku huyo wa Mkoa alieleza zaidi kuwa mfuko wa Bima ya Afya ndio mfuko sahihi kwa kutoa huduma za afya kwa jamii na viongozi wote wanaosimamia huduma za afya ni lazima waondokane na tabia ya kunung’unika na badala yake wanatakiwa kuona umuhimu wa kwenda NHIF kukopa mikopo ambayo inaleta faraja kwa wananchi na si vinginevyo.

Kwa upande wake mganga mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt. Daniel Malekela ameeleza kuwa mpango mzuri wa NHIF wa kutoa mikopo hiyo kwa wadau wa afya zikiwemo halmashauri za Wilaya na manispaa utaweza kuboresha zaidi huduma hiyo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo ya kutolea huduma kwa wagonjwa.

Naye Meneja wa NHIF Mkoa wa Ruvuma  Silvery Mgonza mapema akitoa ufafanuzi juu ya mradi huo na utaratibu wa utoaji mikopo ya vifaa tiba,ukarabati majengo na dawa kwa vituo vya kutolea huduma za matibabu alisema kuwa lengo kubwa ni kuhakikisha kuwa wanachama wa mfuko huo wanapaatiwa huduma bora zaidi pale wanapohitaji kwenda kupata tiba.

Alisema kuwa NHIF imejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa wateja wake wanapata huduma ya tiba kwenye vituo mbalimbali vya kutolea huduma za tiba bila kuwepo manung’uniko ya aina yeyote hivyo amewahimiza viongozi mbalimbali wa taasisi zinazotoa huduma za afya kuona umuhimu wa kuwekeza kwa kuingia mkataba na mfuko huo kwa lengo la kubolesha huduma zinazotolewa kwa jamii inayowazunguka.

Kwa upande wao baadhi ya wenye vituo vya kutolea huduma za tiba wameupongeza mfuko huo kwa kutoa huduma nzuri kwa jamii ambapo wameahidi kuchukuwa hatua mara moja za kujiunga na mradi huo wa mikopo hiyo.

Akichangia mada mkurugenzi wa seven pharmacy Steven Ngonyani alisema kuwa mpango huo wa mfuko wa  bima ya afya wa kuwakopesha wadau vifaa tiba ukarabati wa majengo na dawa kwa vituo vya kutolea huduma za matibabu utawasaidia kwa kiasi kikubwa kwani utaweza kupunguza kero nyingi zilizopo kwenye vituo vyao vya kutolea huduma.

MWISHO.

Chapisha Maoni

 
Top