0
Na Gideon Mwakanosya-Songea.

WANANCHI wa vijiji  vilivyopo katika Kata za Matimila, Mkongotema wilayani songea na Kata ya Lilambo  Manispaa ya Songea wamenufaika  na Elimu ya Sheria za ardhi  namba 5 na namba 4 za mwaka 1999 ambazo  zimeweza kuwajengea uwezo namna ya kumiliki ardhi yao kwa kuepusha migogogro iliyokuwa ikijitokeza mara kwa mara.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na asasi isiyo ya kiserikali ya Songea WOMEN MOVEMENT ON DEVELOPMENT (SOMOWODE) ambayo ilikuwa kwenye zoezi la ufuatiliaji juu ya mafunzo yaliyokuwa yametolewa  ambayo yalifadhiliwa na THE FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY. “FCS”ya jijini Dar es salaam.

Moses Nyoni mwenyekiti wa baraza la usuruhishi la kata ya Matimila alisema kuwa baada ya wanavijiji hivyo kupata mafunzo ya elimu ya sheria za ardhi namba 5 na 4 ya mwaka 1999 wamefanikiwa kutatua migogoro midogomidogo iliyokuwepo hapo awali.

Nyoni alisema kuwa katika kipindi cha nyuma vijiji vilivyopo kwenye kata vilikuwa na migogoro ya mipaka pamoja na wananchi pia kwenye maeneo ya mashamba yao walikuwa wanalalamikiana kuingilia mipaka jambo ambalo kwa sasa limekwisha hivyo ameishukuru asasi isiyo ya kiserikali kwa jitihada iliyofanya kwa kutoa mafunzo ambayo yameweza kuwapa uwezo wa kujua sheria za ardhi.


Anastas Komba katibu wa baraza la ardhi la kata hiyo alieleza kuwa  kutokana na asasi ya SOMOWODE kutoa elimu hiyo wananchi wamefahamu haki za msingi za kumiliki ardhi kwa mfano akimuazimisha mtu shamba hatakiwi kumiliki zaidi ya miaka mitatu na hapaswi kupanda mazao ya kudumu.

Kwa upande wake kaimu afisa mtendaji wa kata ya Mkongotema Polycarp Malekela akitoa taarifa kwa wajumbe wa kamati ya ufuatiliaji ya SOMOWODE alisema kuwa wananchi wa vijiji vya kata hiyo wameshapata elimu ya kutosha ya sheria ya ardhi ya namba 5 na namba 4  na imebainika kuwa hapo awali wananchi wengi walikuwa hawana hati miliki za kimila kutokana na kuwa na uelewa mdogo wa sheria ya ardhi.

Naye  Lotari Gama mkazi wa kata ya Lilambo alisema kuwa wajumbe wa baraza la usuruhishi wa ardhi la kata hiyo baada ya kupatiwa mafunzo hayo wamekuwa ni msaada mkubwa kwa wananchi ambao hapo awali walikuwa na malalamiko  ya mipaka ya maeneo ya mashamba yao ambao kwa sasa hivi malalamiko hayo yameshafanyiwa kazi na wenyewe wameridhika baada ya kuzielewa sheria hizo za ardhi.

Hata hivyo mwenyekiti  wa asasi isiyo ya kiserikali ya SOMOWODE Grace Mbunda aliwaeleza wajumbe kuwa SOMOWODE imedhamilia kutoa elimu hiyo kwa jamii ya watu waishio vijijini kuhusu sheria ya ardhi ya vijiji namba 5 ya mwaka 1999 kwa kuwa wananchi walio wengi hawaifahamu vizuri sheria hiyo na serikali haina mpango wowote wa kuwaelimisha wananchi juu ya sheria hiyo.

MWISHO

Chapisha Maoni

 
Top