0


                                        NAIBU WAZIRI WA MAJI AMOS MAKALLA
NA STEPHANO MANGO, SONGEA
NAIBU Waziri wa Maji Amos Makala ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la mvomero kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) ameonya vitendo vya baadhi ya watu wanaojihusisha na uharibifu wa mazingira  kwa kukata miti ovyo sambamba na hufanyaji wa shughuli za kilimo kwenye vyanzo vya maji kuacha mara moja kwani vitendo hivyo vinachangia kuwepo kwa ukame na kusababisha kukosekana kwa maji.

Hayo ameyasema jana wakati akihutubia wananchi wa watarafa ya Madaba katika halmashauri ya Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma ambapo yupo mkoani humo kwa ziara ya siku nne kutembelea na kuzindua miradi ya maji katika halmashauri nne ambazo ni Namtumbo,Mbinga,Songea vijijini na halmashauri ya manispaa ya Songea.

Alisema kuwa kuna umuhimu wa vijana kupewa elimu juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji na madhara yake hivyo ni jukumu la halmashauri husika kuendelea kuelimisha faida za utunzaji wa mazingira ili maji yaendelee kuwepo na wananchi waweze kufaidika na miradi ya maji inayotekelezwa na serikali.

Awali akizindua mradi wa maji ya mtiririko katika vijiji viwili vya Magingo na Mkongotema vilivyopo halmashauri ya Wilaya ya Songea Makala alisema kuwa serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa kwenye miradi hivyo ni vyema jumuia za maji zilizoundwa zikasimamia miradi hiyo kwa wananchi kuchangia kiasi kidogo cha fedha ambazo zitasaidia kufanyia ukarabati pindi miundombinu hiyo ya maji itakapo haribika badala ya kusubiri serikali itoe fedha kwaajiri ya kukarabati.


Aidha aliwataka wananchi watambue kuwa miradi yote inayotekelezwa mijini na vijijini ni utekelezaji wa ilani wa chama cha mapinduzi hivyo ni wazi kabisa kuwa serikali yao inawajari na kuwataka wananchi wawabeze wale wanaosema serikali yao haijafanya chochote huku wanaona mafanikio yanayofanywa na wanaitumia miradi hiyo.

Kwa upande wake mweneyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Songea vijijini Rajab Mtiula amempongeza naibu waziri huyo kwa kuwasaidia fedha ambazo zimesaidia kupata mradi wa maji ya mtiririko na kwamba utawasaidia wananchi wa vijiji hivyo viwiwli ambao mwanzo walikuwa wakichota maji toka mtoni jambo ambalo lilikuwa ni kero kubwa.


Nae kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya hiyo Wenisalia Swai akisoma taarifa ya mradi huo wa maji ya mtiririko kwa naibu waziri wa maji alisema kuwa mradi huo hadi kukamilika utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.60 na utahudumia wanachi zaidi ya 5000 na kwamba tayari wameshaweka mikakati ya kuhakikisha mradi huo unakuwa endelevu wataendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya maji.

Nao baadhi ya wananchi wa vijiji hivyo wakiongea na mwandishi wa gazeti hili wameishukuru serikali kwa kuwaletea mradi huo wa maji ambao wanaimani utawapunguzia kero ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji jambo ambalo lilikuwa linawakwamisha kwenye shughuli zao za kila siku za kujileta maendelao ndani ya famila zao.
MWISHO.

Chapisha Maoni

 
Top