0



MBUNGE WA SONGEA MJINI DKT EMMANUEL NCHIMBI AKIZUNGUMZA KWENYE MOJA YA MIKUTANO YAKE



NA STEPHANO MANGO,SONGEA

MBUNGE wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Emmanuel Nchimbi amewaacha njia panda wapiga kura wake baada ya kuwaeleza taarifa ya  utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Ccm kwa kipindi cha miaka 10 katika jimbo hilo na kuwaambia huenda kuwa hata gombea tena katika Jimbo hilo



Dkt Nchimbi akizungumza jana na viongozi wa mashina, matawi, kata ,madiwani,wenyeviti wa mitaa, mabalozi na wa Wilaya ya Songea mjini kwenye uwanja wa michezo wa Majimaji mjini hapa alisema ni ukweli uliowazi kuwa tumepata mafanikio makubwa katika maendeleo ya jimbo kwenye sekta ya elimu,maji,afya,barabara na ujenzi,kilimo na ushirika,mifugo na uvuvi,ardhi na maliasili,umeme,mawasiliano,biashara na masoko,utawala bora na michezo



“Nimepongezwa sana kwa mafanikio makubwa tuliyoyapa lakini naomba nikiri wazi kuwa kazi hizi sikuzifanya peke yangu, hivyo kwa heshima kubwa naomba niwashukuru nyie viongozi wenzangu wa chama na serikali mliopo hapa na wale ambao wamepita ndani ya miaka hii kumi ya uongozi wangu kwani walikuwa chachu ya maendeleo,hata  hivyo  sikusudii kugombea tena jimbo la Songea” alisema Nchimbi



Alisema kuwa katika kipindi hiko cha miaka kumi Jimbo la Songea Mjini lilipata heshima kubwa sana kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete kwa kumuamini na kumteua kushika Unaibu Uwaziri katika Wizara mbalimbali  na baadae uwaziri kamili katika wizara mbili tofauti lakini pia amekuwa chachu na kimbilio langu wakati wote ambapo nilikwama katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya jimbo la Songea, hivyo namshukuru sana yeye binafsi na serikali yake kwa imani na mapendo yake kwa wananchi wa Songea Mjini



Alisema kuwa nimepata wakati mgumu sana kuyasema maneno haya lakini nimeyasema kwani ilani na ahadi zangu binafsi nimezitekeleza kwa ukamilifu na nyie wenyewe ni mashahidi kwani yote niliyoyasema hapa huko kwenye maeneo yenu mnayaona hivyo nataka niondoke nikiwa kifua mbele



Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi hao walionyesha masikitiko makubwa sana na maneno aliyoyasema Dkt Nchimbi ambayo kisiasa yalionyesha kuwa ndio anawaaga kutogombea jimbo hilo ingawa pia hajasema anakwenda wapi.



Kwa upande wake Kada wa chama hicho Alfonce Haule alisema kuwa hatua hiyo imewachanganya sana na imewaacha njia panda wapigakura wa Jimbo hilo hivyo wazee wamejipanga kwenda kuzungumza nae ili aweze kuja kugombea tena kwani mchango wake kwa maendeleo ya jimbo hilo ni mkubwa sana.



Haule alisema kuwa Dkt Nchimbi uongozi wake tuliuzoea na hata alipokosea tulimshauri  na alijirekebisha sasa leo ghafla anatuacha na nani na huyo anayekuja mpaka tutakapomzoea na kumsahihisha atakapokosea itakuwa kasi ya maendeleo imesimama kwa muda mrefu



Alisema kuwa timu ya wazee iliyoundwa kwenda kumshauri arudi ni timu makini na tunaamini siku ya jumapili juni 28 mwaka huu itatuletea majibu ili tujue namna ya kujipanga ingawa tunaamini kuwa Dkt Nchimbi ni msikivu ataelewa nia na kilio cha wanasongea



Naye kada mmoja wa Ccm kutoka Wilaya ya Nyasa  akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu ya mkononi ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema kuwa Dkt Nchimbi Juni 19 na juni 20 alikuwa Wilayani humo na alikutana na makundi mbalimbali na kuwakaribisha kwenye misa ya shukrani kwa Mungu kwa jinsi alivyomlinda kwa miaka yote ya maisha yake ambapo misa  hiyo ilifanyika nyumbani kwake katika  kijiji cha Mbaha wilayani Nyasa.



Kada huyo alisema kitendo hicho kimewashtua viongozi mbalimbali wa chama na wananchi kwani hawaelewi nia yake kwasababu amewaita na amesali nao na amekula nao  kisha akawashukuru kwa kuja kwao kujumuika nae kwenye hafla hiyo bila kueleza nia kama ana nia yoyote, kumekuwepo na shinikizo kubwa kutoka makundi mbalimbali ya kijamii wilayani Nyasa  la kutaka agombee jimbo la Nyasa kwa kuamini kuwa kasi ya Maendeleo iliyopatikana Songea itapatikana pia Nyasa.



 Awali duru za kisiasa zilionyesha kuwa miongoni mwa makada vijana ambao walikuwa wanatajwa sana  kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya Urais Dkt Nchimbi alikuwa ni mmojawapo lakini mpaka leo hajajitokeza kuchukua fomu na wala kusema jambo lolote



Hata hivyo taarifa kutoka kwa mtu wa karibu naye ambaye ameomba jina lake lihifadhiwe amesema kuwa Dkt Nchimbi amekwisha kaa vikao na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali mjini Songea na kuwashukuru kwa kipindi chake cha miaka kumi ya ubunge, ingawa ajasema chochote kuelekea kwenye uchaguzi wa mwaka huu Dr Nchimbi anafahamika sana kwa uwezo wake wa kutunza siri moyoni kwa hiyo lolote linaweza kutokea anaweza kugombea Nyasa au anaweza kugombea Songea au hata Urais siku zinakaribia kitendawili kitajitegua.

MWISHO



Chapisha Maoni

 
Top