0


MBUNGE WA JIMBO LA NAMTUMBO VITA KAWAWA AKIZUNGUMZA KWENYE MOJA YA MIKUTANO YAKE

NA STEPHANO MANGO,NAMTUMBO

MAKADA 14 wa Chama cha Mapinduzi (Ccm) wakiwemo waliowahi kuwa vigogo Serikalini wanatajwa kuwania ubunge kwenye Jimbo la uchaguzi la Namtumbo mkoani Ruvuma ambalo kwa sasa linawakilishwa na Vita Mfaume Kawawa ambaye amewakilishi kwa vipindi  viwili vya  miaka 10  hadisasa

Habari zilizopatikana mjini hapa jana na kuthibitishwa na Katibu wa Cccm wa Wilaya ya Namtumbo Mohamed Azizi zilisema kuwa baadhi ya makada hao wametangaza nia na wengine wameshaanza kupita pita kwenye kata na vijiji vya Jimbo hilo kwa minajiri ya kujitambulisha kwa wananchi na wapiga kura wa chama hicho ni pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi na balozi mstaafu wa Japan Salome Sijaona

Aziz alisema wengine ni aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Barabara za Vijijini Taifa Mhandisi Vintan Kilowoko, Mkurugenzi wa shirika la madini Nchini(Stamico) Mhandisi Edwin Ngonyani, Afisa Masoko wa Manispaa ya Songea Salum Homera, Afisa wa Wizara ya Maji Mwinyiheri Ndimbo, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Zainab Mbillo na Charles Fussi ambaye anafanya kazi Idara ya Usalama wa Taifa jijini Dar Es Salaam

Aliwataja wengine kuwa ni Oraph Nchimbi,Mrisho Mpoto ambaye ni msanii, Mussa Chowo ambaye anafanya kazi Tanesko Makao Makuu,Alphelio Nchimbi,Joseph Mbawala ambaye ni Afisa Elimu Mstaafu,wengine ni Edwin Millinga anafanya kazi Ccm Makao Makuu na Mwalimu wa Sekondari ya Utwango wilaya ya Namtumbo Shaib Majariwa

Alifafanua kuwa chama bado hakijatangaza rasmi muda wa kuanza kampeni za ubunge kutokana na kanuni na sheria zilizopo hivyo anawataadharisha watia nia hao ambao wanatajwa tajwa na wapambe wao kutojihusisha na siasa chafu kwani mbunge aliyepo bado anatekeleza ilani ya chama ya mwaka 2010

Duru za kisiasa jimboni humo zinaonyesha kuwa tayari kambi za wagombea zimeundwa na zinafanya kampeni za chini kwa chini kwa kupita kwa mabalozi wa mashina, viongozi wa matawi, wenyeviti wa vijiji na kata na kwa wazee maarufu ili kuombwa kuungwa mkono wakati ukifika

Baadhi ya wachambuzi wa Siasa jimboni humo waliozungumza na gazeti hili walisema kuwa kujitokeza kwa wingi watia nia hao kuna onyesha ninamna gani kipindi cha Uongozi wa Vita Kawawa ulivyokuwa na mapungufu katika masuala ya maendeleo ya jimbo hilo

Salum Brash alisema kuwa awali wananchi walikuwa wanamategemeo makubwa sana ya kupata maendeleo lakini wamekosa ushirikiano kutoka kwa mbunge wao na hasa kuhusu kilimo cha zao la Tumbaku ambalo kimsingi ndio uti wa uchumi wa wilaya hiyo ya Namtumbo

Brash alisema kuwa Vita Kawawa aliingia na Rais wa awamu ya nne ya Jakaya Kikwete hivyo awamu ya tano ni lazima apatikane mwakilishi mwinge atakaye endeleza mafanikio madogo yaliyopatikana kwenye vipindi vyake viwili vya uwakilishi wa jimbo hilo

Jitihada za kumpa Mbunge wa Jimbo hilo Vita Kawawa ili gazeti lipate msimamo kama atachukua fomu ya kugombea tena ubunge na kueleza mafanikio aliyoyapata hazikuzaa matunda kwani simu yake ya kiganjani ilipopigwa haikupatikana
MWISHO





Chapisha Maoni

 
Top