Na Stephano Mango, Mbinga.
MAGARI mawili yaliyokuwa katika msafara wa kampeni wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) katika kijiji cha Mtua, kata ya Mpepai wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma
yameharibiwa vibaya baada ya watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuvamia msafara huo, na kurusha mawe huku
watu waliokuwemo ndani ya magari hayo nao wakinusurika kuumia vibaya.
Tukio hilo lilitokea Septemba 19 mwaka huu majira ya jioni, ambapo
Katibu wa CCM wilaya ya Mbinga, Zainabu Chinowa ndiye aliyekuwa akiongoza
msafara wa kampeni wa chama hicho katika kata ya Mpepai na vijiji vyake kwa
lengo la kumnadi mgombea wa nafasi ya udiwani kupitia tiketi ya chama hicho,
Benedict Ngwenya.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Chinowa alisema kuwa
wakati wakiwa barabarani wanarudi wakitokea katika kijiji cha Mtua ghafla
waliona magogo makubwa ya miti yakiwa yamewekwa barabarani, ili kuzuia wasiweze
kupita na baadaye walipojaribu kuyatoa ndipo kundi la vijana lilijitokeza na
kuanza kuwarushia mawe, ambayo yaliweza kuharibu na kuvunja vioo vya magari
hayo yaliyokuwa katika msafara huo.
“Kwa kweli tumenusurika kuumizwa vibaya, gari letu la chama
limevunjwa kioo cha ubavuni na gari lingine moja ambalo ni la mgombea wetu nalo
limevunjwa vunjwa karibu vioo vyote, tumeripoti Polisi ili hatua ziweze
kuchukuliwa”, alisema Chinowa.
Chinowa alieleza kuwa waliohusika katika tukio hilo, ni wafuasi wa
CHADEMA ambapo wakati wanafanya unyama huo, wengine walionekana wakiwa
wamevalia sare za chama hicho.
Mwandishi wa gazeti hili ameshuhudia magari hayo yakiwa kituo cha
Polisi wilaya ya Mbinga, ambapo gari la CCM wilaya lenye namba za usajili T 545
BEW aina ya Landcruiser Hardtop limevunjwa kioo cha ubavuni upande wa kushoto
na lingine aina ya Landrover Discover, lenye namba T 797 AEN nalo limevunnjwa
vunjwa vioo kwa mawe hayo ambayo yalikuwa yakirushwa.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Revocatus Malimi
alipohojiwa na waandishi wa habari alisema kuwa taarifa kamili bado
hazijamfikia ofisini kwake na kwamba, anaendelea kufanya mawasiliano na Mkuu wa
Polisi wilaya ya Mbinga ili aweze kupata undani wa tukio hilo.
Chapisha Maoni