0

MKE WA MGOMBEA URAIS EDWARD LOWASSA , MAMA REGINA LOWASSA
MGOMBEA WA UBUNGE JIMBO LA SONGEA MJINI JOSEPH FUIME AKIENDELEA KUWAOMBA KURA WANANCHI


NA STEPHANO MANGO, SONGEA



MKE wa mgombea Urais kupitia umoja wa Katiba ya Wananchi(UKAWA) Regina Lowassa anatarajia kuhutubia maelfu ya wananchi wa Manispaa ya Songea na vitongoji vyake kesho(leo) kwenye kiwanja cha wazi kilichopo kata ya Bombambili Katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea



Akizungumza na waandishi wa habari jana Ofisini kwake Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema Mkoa wa Ruvuma (Bawacha) Mariam Mtamike alisema kuwa Regina Lowassa akiwa ameambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Bawacha Taifa Kunti Majara na viongozi wengine toka makao makuu ya Chadema atafanya mkutano mkubwa kuanzia majira ya saa 5:00 asubuhi mpaka majira ya saa 11:15 na baada ya hapo ataelekea Mkoani Mbeya kwenye mikutano mingine ya Kampeni



Mtamike alisema kuwa lengo la mkutano huo ni kuwanadi wagombea Urais,Ubunge na Madiwani wa Ukawa na kuzungumza na wanawake wa Wilaya ya Songea wawe na ujasiri wa kufanya mabadiliko ya kuwachagua wagombea hao ili kuyafikia malengo stahiki



Alisema kuwa Chadema Mkoa wa Ruvuma wamejipanga kikamilifu katika kuhakikisha kuwa ushindi wa kishindo unapatikana kwa wagombea wa ukawa kwani kwasasa wanawake wanaendelea na mikakati ya ushindi ikiwemo kupita nyumba kwa nyumba kuwanadi wagombea wao na kuwahamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi siku ya uchaguzi Octoba 25 mwaka huu na kuwachagua wagombea wa Ukawa kwa nafasi ya Udiwani, Ubunge na Urais



“Naziomba mamlaka zinazohusika ikiwemo Tume ya Taifa ya Uchaguzi iwaache wananchi wapige kura kwa uhuru ili watimize haki yao ya kimsingi ya kupiga kura kwa wagombea ambao wanawahitaji kwani kuendelea kusuka hujuma kutaleta vurugu ambazo zitaharibu amani, na hata haki ya wapiga kura hao kulinda kura zao isichezewe” alisema Mtamike



Alisema kuwa wananchi wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kwenye mkutano huo ili waweze kupata ujasiri wa kupiga kura na kulinda kura zao siku ya uchaguzi ili kuweza kufanya mabadiliko ya dhati ya kiuongozi mwaka huu



Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) John Mwankina alisema kuwa kuna taarifa za uchakachuaji ambazo wamezibaini na kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuzifanyia kazi haraka iwezekanavyo ili kuufanya uchaguzi uwe wa haki



Mwankina alisema kuwa idadi halali ya wapiga kura jimbo la uchaguzi la Songea Mjini ni 127,719 lakini imeonyesha kuwa wapigakura waliozidi ni 1122 hivyo tumeiandikia tume barua yenye kumbukumbu namba CDM/SMJ/10/2015/17 ya tarehe 13/10/2015  ili iweze kutoa ufafanuzi wa kina wa idadi halali ya waliojiandikishe kupiga kura ili kuondoa dosari katika uchaguzi wa jimbo hilo



Alisema kuwa Chama cha Mapinduzi kwa kushirikiana na Serikali imekuwa ikihangaika kuwafanyia hujuma mbalimbali wagombea wa Ukawa wa nafasi ya Udiwani na Ubunge hali ambayo inatutia shaka na kuwapa hofu wananchi kwenye mchakato mzima wa kampeni na kuelekea uchaguzi

MWISHO







Chapisha Maoni

 
Top