0
        WAENDESHA BODA WAKIWA KWENYE KIJIWE CHAO CHA KUSAKA ABIRIA
Na Julius Konala,Songea

ZAIDI ya waendesha bodaboda 100 wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wamejiunga na mfuko wa taifa wa hifadhi ya jamii(NSSF) mkoani Ruvuma.

Hayo yalisemwa jana na Meneja wa mfuko wa taifa wa hifadhi ya jamii wa mkoa wa Ruvuma Dominic Mbwette,wakati alipokuwa akiongea na gazeti hili ofisini kwake mjini Songea.

Mbwette alisema kuwa shirika lake limeamua kuendesha semina ya siku moja kwa waendesha bodaboda hao ili waweze kujiunga na mfuko wa mafao ya matibabu na kuumia kazini kwa kuwa wao ndio wahanga wakubwa.

Alisema kuwa kiingilio kwa ajili ya mfuko huo ni shilingi 20,000 ambazo zitasaidia kuwawezesha kutibiwa katika hospitali mbalimbali hapa nchini huku akidai kuwa shirika hilo linatarajia kuwafikia waendesha bodaboda wa wilaya ya Namtumbo,Songea,Madaba,Tunduru na Nyasa.

Meneja huyo pia amewaomba wajasiriamali mbalimbali wakiwemo wakulima kujiunga na mfuko huo wa  NSSF  ili waweze kupata mafao mbalimbali ya matibabu,mafao ya uzazi,mafao ya kuumia kazini na msaadawa mazishi ili iweze kuwasaidia pindi wanapopatwa na matatizo.

Alisema kuwa tayari shirika lake limekwisha toa elimu hiyo kwa wanafunzi wa chuo kikuu cha Udaktari cha st.Augustine Peramiho,waendesha bodaboda na kundi la jumuia ya umoja wa wanawake wa CCM mjini Songea.

Kwa upande wao baadhi ya waendesha bodaboda hao wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti walisema kuwa wameamua kujiunga na mfuko huo baada ya kuona kuwa wao ndio wahanga wakubwa wa kupata ajali bila ya kuwa na msaada wowote wa matibabu.

MWISHO


Chapisha Maoni

 
Top