0
                   MKURUGENZI WA MADABA ROBART MAGENI
 
NA STEPHANO MANGO,SONGEA
HALMASHAURI mpya ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma imejipanga kikamilifu kupima viwanja kwa ajiri ya ujenzi wa ofisi za makao makuu ya Wilaya hiyo na viwanja vya makazi ya wananchi kwa kufuata taratibu za mipango miji na kuufanya mji huo kuwa wa kisasa zaidi

Akizungumza na gazeti hili jana Ofisini kwake Afisa Ardhi wa Halmashauri hiyo Leonsi Mtalemwa  alisema kuwa halmashauri inatarajia kuanza mchakato wa ujenzi wa nyumba za watumishi na kwa kuanzia mpango huo utaanza na ujenzi wa nyumba za wakuu wa idara ambao wanastahili kupewa nyumba za kuishi katika utumishi wao

Mtalemwa alisema kuwa tayari viwanja 600 vimeshapimwa likiwemo stendi ya mabasi ambapo wananchi waliopewa viwanja katika eneo hilo wametakiwa kukamilisha ujenzi wa vibanda vya biashara kama mpango ulivyowekwa na kufanya matumizi bora ya ardhi yanatekelezwa

Alisema kuwa kuna eneo jingine ambalo linatakiwa lipimwe viwanja bado halijalipwa fidia hivyo jitihada zinaendelea ili kupata fedha na kulipa fidia ili upimaji  wa viwanja uendelee kwa ajiri ya ujenzi wa makao makuu ya Hakmashauri, viwanja kwa ajiri ya ujenzi wa nyumba mbalimbali na maeneo ya kuabudia na kuzikana

Naye Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo Prosper Luambano alisema kuwa kwasasa Halmashauri inakarabati jengo la kituo cha habari kwa wakulima ili kuwezesha ofisi ya watumishi wa kada mbalimbali kuanzia kazi zao hapo wakati hatua zingine za ujenzi wa ofisi za kutumu zikiendelea

Luambano alisema kuwa Halmashauri imepeleka ombi maalum Hazina ili kuwezesha upatikanaji wa gari la Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya,ujenzi wa nyumba yake pamoja na upatikanaji wa umeme na maji kwenye makazi ya mkurugenzi huyo

Alisema kuwa Halmashauri hiyo inatarajia kuanza mchakato wa ujenzi wa jengo la makao makuu yake ambalo linatarajiwa kujengwa kwenye maeneo mapya yatakayopimwa vizuri upande wa barabara ya Songea-Njombe ambapo maombi ya mpango huo mahsusi umejumlishwa kwenye mpango wa bajeti wa Halmashauri kwa mwaka 2016/17 na kuendelea hadi ujenzi utakapokamilika
MWISHO

Chapisha Maoni

 
Top