0


NA STEPHANO MANGO,SONGEA

CHUO cha ufundi stadi cha Top one Inn VTC katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma kimewazawadia wahitimu nane vyerehani  vyenye thamani ya shilingi milioni nne kwa ajili ya kuwasaidia kujiajiri kwa kufungua viwanda vidogo vidogo.

 Zawadi hizo zilitolewa juzi na mkurugenzi wa chuo hicho Pascal Msigwa,kwenye mahafali ya kumi ya chuo hicho yaliyofanyika chuoni hapo na kuhudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo wazazi wa wahitimu,walimu na wanafunzi.

Msigwa alisema kuwa chuo chake kimeamua kutoa zawadi ya vyerehani kwa wahitimu hao ambao ni Yatima ili waweze kwenda kufungua ofisi zao kwa lengo la kujiingizia kipato na kutoa huduma katika jamii inayowazunguka huku akitoa wito kwa wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao kujiunga na vyuo vya ufundi stadi kwa lengo la kupunguza tatizo la ajira kwa vijana badala ya kuwaacha wakizurura ovyo mitaani.

Afisa elimu sekondari Manispaa ya Songea mkoani humo,Leo Mapunda ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo amewapongeza wahitimu hao na kuwataka kutumia elimu na ujuzi walioupata kwa ajili ya kujiletea maendeleo kwa kuanzisha viwanda vidogo vidogo.

Akizungumza katika mahafali hayo,mkuu wa chuo cha Top one Inn VTC Manispaa ya Songea mkoani humo Edwin Ndunguru,alisema kuwa chuo chake kilianzishwa mwaka 2007 kikiwa na wanachuo 40 kwa fani  za Hotel,utalii,uhazili na kompyuta ambapo hadi kufikia mwaka 2014 jumla ya wahitimu 857 wamehitimu katika chuo hicho huku akidai kuwa kinakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa eneo na kushindwa kuendeleza  shughuli nyingine za chuo hicho.

Kwa upande wao wahitimu hao Eva Nikata,Asante Kabata na Winess Soko wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili,wameushukuru uongozi wa chuo hicho kwa kuwasaidia kupata ujuzi katika kipindi chote walichokuwepo chuoni hapo pamoja na zawadi ya vyerehani ambapo wamedai vitawasaidia kujiajiri wenyewe kwa kufungua viwanda vidogo vidogo.

Aidha mgeni rasmi katika mahafali hayo Afisa elimu sekondari Manispaa ya Songea Mwalimu Leo Mapunda,aliwatunikia vyeti vya fani mbalimbali wahitimu 38 wa chuo hicho cha Top one inn cha mjini Songea.

MWISHO

Chapisha Maoni

 
Top