1
                                      RPC RUVUMA ZUBERI MWOMBEZI

NA STEPHANO MANGO,SONGEA

JESHI la polisi mkoani Ruvuma limemtia mbaroni Kassim Millinga (52) mkazi wa Lizaboni Manispaa ya Songea kwa tuhuma za kuwabaka wanafunzi watatu(3) wanaosoma darasa la sita katika shule ya msingi ya Kibulang`oma iliyopo Manispaa hiyo.

Akizungumza na gazeti hili jana ofisini kwake Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma Zuberi Mwombeji alisema kuwa tukio hilo limetokea kwa nyakati tofauti katika eneo la Lizaboni jirani na shule wanayosoma wanafunzi hao ambao majina yao yamehifadhiwa wenye umri wa miaka 12 kila mmoja.

Alisema kuwa Millinga ambaye pia anafanya kazi ya ulinzi kwenye kampuni ya Ulinzi Ilonjezi ya mjini Songea anatuhumiwa kuwa kwa nyakati tofauti tangu mwaka jana amekuwa akiwarubuni wanafunzi hao kwa kuwapa pesa, chakula na nguo kisha kuwafanyia kitendo cha kinyama kwenye nyumba anayoishi na kuwalazimisha kutosema kwa mtu yeyote kuhusiana na vitendo hivyo anavyowafanyia.

Alifafanua zaidi kuwa januari 26 mwaka hu majira ya saa nane mchana wanafunzi hao wakiwa kwenye eneo la shule walikutwa na Mwalimu mmoja wa shule hiyo wakiwa wanagombania shilingi 1500 ambazo inadaiwa walikuwa wamepewa na Millinga na alipoona wanafunzi hao wanaendelea kugombaniana fedha hizo alilazimika kusimama ili aweze kufahamu chanzo ni nini.

Alieleza zaidi kuwa baadaye aliwauliza sababu ambayo inawafanya wagombee hizo fedha jambo ambalo lilimlazimu aendelee kuwabana ili wamueleze wamepata wapi fedha hizo ndipo wanafunzi hao walimjuza Mwalimu wao jinsi walivyofanyiwa na Milinga na kwamba fedha hiyo alikuwa amewapa baada ya mmoja wao kufanya mapenzi naye.

Kamanda Mwombeji alieleza zaidi kuwa inadaiwa kuwa wanafunzi hao walimweleza Mwalimu wao kuwa tangu mwaka jana wamekuwa wakifanya mapenzi na Millinga kwa nyakati tofauti ambaye amekuwa akiwapa vitu mbalimbali zikiwemo pesa, nguo, na chakula jambo ambalo Mwalimu huyo lilimshtua na kumlazimu kutoa taarifa kwa uongozi wa Shule kisha taarifa hizo zilifikishwa kwenye kituo kikuu cha Songea.

Alisema kuwa Polisi baada ya kupata taarifa ya tukio hilo walimsaka mtuhumiwa Millinga na baadaye walifanikiwa kumkamata ambapo katika mahojiano ya awali alikili kufanya mapenzi na wanafunzi hao ambao walikuwa wanaenda kufanya kazi ya kumpigia deki chumba cha nyumba anayoishi.

Alisema kuwa uchunguzi wa kitaalamu bado unaendelea na muda wowote kuanzia sasa ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili.

MWISHO

Chapisha Maoni

 
Top