NA STEPHANO MANGO,SONGEA
JESHI la Polisi Mkoa wa Ruvuma linawashikilia mkazi mmoja wa Kijiji cha Mbangamawe kata ya
Gumbiro Wilayani Songea Musa Moyo (40) kwa tuhuma za kukutwa akiwa anauza nyama
ya Mbwa
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Revocatus Malimi amelitaja tukio la kwanza limetokea jana majira ya saa 10:30 jioni huko katika kijiji cha Mbangamawe ambako inadaiwa Moyo alikamatwa na Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho akiwa anauza nyama hiyo ya Mbwa
Malimi alisema kuwa taarifa zaidi juu ya tukio hilo kutoka
kwa Afisa Mtendaji wa kijiji hicho Theopista Komba zinadai kuwa siku hiyo ya
tukio akiwa nyumbani kwake alipokea taarifa za siri kutoka kwa raia wema kuwa
Moyo anafanya biashara ya kuuza nyama ya Mbwa kwa matumizi ya binadamu
Alisema kuwa kufuatia taarifa hizo Mtendaji wa Kijiji hicho
alilazimika kufuatilia kwa kina tukio hilo na baadae alilazimika kwenda kwa mhusika
ambako alijifanya mteja na anahitaji kununua nyama hiyo kwa ajiri ya kitoweo
cha siku hiyo
Alifafanua kuwa awali Moyo alimjibu Mtendaji huyo kuwa nyama
ilikuwa imeisha hivyo yeye amechelewa kupata kitoweo hicho,baada ya kupata
majibu hayo Afisa Mtendaji aliendelea kumbembeleza ili amuuzie nyama hiyo kwani
nyumbani kwake hakuwa na mboga siku hiyo na kwamba alikuwa anaitegemea nyama
hiyo
Alieleza zaidi kuwa baada ya kuombwa sana, Moyo alikubali
kumuuzia Komba nyama kidogo iliyokuwa imebaki ndipo Mtendaji huyo alipomkamata
na nyama hiyo iliyokuwa imekaushwa na kukatwa vipande vipande
Malimi ambaye pia ni Afisa upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa
wa Ruvuma alifafanua kuwa Moyo baadae alifikishwa katika Kituo Kikuu cha Polisi
Mjini Songea na kufanyiwa mahojiano ya kina ambapo mtuhumiwa huyo alikiri kuwa
nyama hiyo ni ya Mbwa ambaye alikuwa amemchinja siku moja kabla ya kukamatwa na
alidai kuwa nyama hiyo ilikuwa ni kwa ajiri ya matumizi yake tuu ambayo mara
kwa mara familia yake imekuwa ikitumia kitoweo hicho na kwamba kuna baadhi ya
watu wachache walikuwa wamekula nyama hiyo baada ya kuuziwa bila wao kujua
kwani aliwaambia kuwa hiyo ni nyama ya Polini
Alisema kuwa Polisi walilazimika kuwasiliana na Afisa Mifugo
wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambaye baada ya uchunguzi wake
alithibitisha kuwa kitoweo hicho ni nyama ya Mbwa, ingawa polisi inaendelea
kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na tukio hilo na kwamba kufuatia tukio hilo
Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma limewatahadharisha wananchi wote kuacha mara
moja kununua nyama mitaani
MWISHO
Chapisha Maoni