NA STEPHANO MANGO,NAMTUMBO
JUMUIYA ya
kuhifadhi na matumizi endelevu ya maliasili Mbaran’gandu iliyopo kwenye bunga
ya hifadhi ya wanyama ya Selous katika Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma
imeingia dosari baada ya vijiji wanachama kususia uchaguzi wao kutokana na
madai ya ukiukwaji wa kanuni unaofanya na viongozi waandamizi wa wilaya hiyo
ambapo wamemwomba Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne Maghembe
aingilie kati mgogoro huo ili aweze kutumbua majipu katika jumuiya hiyo muhimu
kiuchumi kwa Wilaya ya Namtumbo na Taifa kiujumla
Akizungumza na
waandishi wa Habari Ofisini kwake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mchomoro Juma
Mhogola alisema kuwa maelekezo ya uchaguzi huo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya
ya Mbarang’andu Wilaya Devid Mgala na Afisa wa Nyamapoli Wilaya hiyo Ernest
Nombo yanachembechembe ya ufisadi licha ya kuwa ni kinyume cha katiba ya
Jumuiya yao
Mhogola alisema
kuwa huwezi kuitisha uchaguzi ambao viongozi wa zamani huenda ukawaweka kando
au wasigombee bila kuitisha mkutano wa hadhara ambao utasoma mapato na matumizi
na kujua mali za jumuiya yao kabla hazijakabidhiwa kwa viongozi wapya kama
kanuni na tararibu za makabidhiano ya mali za jumuiya inavyotakiwa
“Ni miaka zaidi
ya mitatu wanachi hawajapata taarifa yoyote katika mkutano wa hadhara ambao
utaeleza mali za jumuiya na mgao wa fedha
za maendeleo ya kijiji hicho ambao umetokana na tozo mbalimbali kutoka
kwa mwekezaji ambaye anawinda katika hifadhi yao”alisema Mhogole
Alisema jumuiya
ya Mbarang”andu inaundwa na vijiji saba ambavyo ni Kitanda,
Songambele,Nambecha,Likuyusekamaganga,Mchomoro,Kilimasera na Mtelawamwahi kati
ya vijiji hivyo ni vijiji vitatu tu ndivyo vimefanya uchaguzi na vijiji vinne
vimekataa uchaguzi huo kutokana na ukiukwaji wa katiba na hata vijiji ambavyo
vimefanya uchaguzi huo kuna malalamiko mengi sana ambayo yanaukosesha uchaguzi
huo kuwa wa huru na haki
Naye Mhasibu wa
kijiji cha Mchomoro Hassan Likwata alisema kuwa yeye ni mjumbe wa Kamati ya kuchuja
majina ya wagombea katika Kijiji chake lakini alishangaa kuondolewa kwenye
kikao hicho cha uchujaji na Afisa Wanyamapori wa Wilaya Ernest Nombo hali iliyosababisha
kupitisha majina ambayo yalikosa sifa na kuwaacha wenye
sifa hali ambayo ilizua tafrani mpaka uchaguzi kuvurugika
Likwata alisema kuwa
mwanzoni mwa Januari mwaka huu alipokea ugeni ulioongozwa na Nombo ili kujadili
majina ya wagombea 13 waliojaza fomu ya kuomba ujumbe wa baraza la Jumuiya hiyo
lakini cha kushangazwa kwenye kikao hicho Nombo akiwa na wagombea wa vijiji
vingine wakatuondoa kwenye kikao na kupitisha majina kumi ya wagombea ambao
kimsingi hawakuwa na sifa ili waende wakapigiwe kura na wananchi na wapatikane
viongozi wa tano kutoka kijiji hicho watakaokwenda kuunda baraza la Wilaya
Alisema kuwa
kutokana na hali hiyo na kashfa nyingine za ubadhirifu wa fedha za
jumuiya,uvunjaji wa katiba na utawala mbovu wa Afisa Wanyamapori huyo ni lazima
mamlaka zinazohusika kumchukulia hatua kwani ameshindwa kutimiza wajibu wake
kwa kushindwa kusimamia maliasili za wilaya hiyo na kwamba amemwomba waziri
mwenye dhamana hiyo Profesa Maghembe kuona umuhimu wa kufika Namtumba na
kusikiliza kero hizo sugu ambazo zinasababisha kuwepo majipu yaliyoiva na
yakisubiri kutumbuliwa
Diwani wa Kata
ya Mchomoro Kassim Nabea akizungumzia mgogoro huo alikiri kutofanyika mkutano
huo wa uchaguzi ambapo alidai kuwa wananchi wamesusia uchaguzi huo kutokana na
kutosomewa mapato na matumizi ya jumuiya hiyo kwa muda mrefu na bila kuwepo
taarifa yoyote
Nabea alisema
kuwa wananchi wanataka ufafanuzi wa fedha zaidi ya milioni 80 za miradi ya
kijiji ambayo inafadhiriwa na jumuiya ya Mbarang’andu baada ya kupokea fedha
hizo kutoka kwenye gawio la mwekezaji anayewinda katika hifadhi ya jumuiya hiyo
Alisema kuwa pia
wananchi wanataka kujua zilipo mali ya jumuiya na kwamba baada ya kuridhishwa
na ufafanuzi wa madai yao ndipo uchaguzi unaweza ukafanyika kwa kuzingatia
kanuni za kutaka majina yote ya wagombea yarudishwe kwa wananchi kasha yapigiwe
kura katika mkutano wa hadhara
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti wananchi wa Vijiji vya Kitanda,Mchomoro, Likuyusekamaganga na
Songambele wamelaani sana kitendo hicho alichofanya Afisa Wanyamapori Nombo cha
kuitisha uchaguzi na kuingilia mamlaka halali za vijiji kwa maslahi yake ,
jambo ambalo linaonyesha wazi ni ubabe na ulevi wa madaraka
Walisema kuwa
jambo hilo linaashiria kuna mkono mrefu ambao unafadhiriwa na majangiri wa
jumuiya hiyo ya Mbarang’andu na watu wasiozitakia mema maliasili zilizopo katika
hifadhi inayoizunguka Selous
Kwa Upande wake
Afisa Wanyamapori wa Wilaya hiyo Ernest Nombo alipotafutwa na waandishi wa
habari ili aweze kujibu tuhuma zinazomkabili alisema kuwa yeye sio msemaji
atafutwe mkurugenzi wa Wilaya hiyo
Juhudi za
kumpata Mkurugenzi wa Wilaya ya Namtumbo Ally Mpenye zilifanikiwa na
alipoulizwa kuhusu mgogoro huo alikiri kuhufahamu na kusema kuwa tayari
amechukua hatua za kusimamisha uchaguzi huo na kwamba anaandaa mikutano ya
hadhara ili kuweza kuzungumza na wananchi ili aweze kupokea kero hizo kwa kina
na kuzichukuria hatua
MWISHO
Chapisha Maoni