WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AKITEMBEA NFRA RUVUMA
MENEJA WA NFRA RUVUMA MORGAN MWAIPAYA AKIFAFANUA JAMBO
NA STEPHANO MANGO,SONGEA
WAZIRI Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa, ameutaka uongozi wa Wakala
wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) hapa nchini, kuhakikisha kwamba
wanajipanga kikamilifu katika kuhakikisha kwamba wakulima wa zao la
mahindi wanapatiwa magunia ya kuhifadhia zao hilo, katika maeneo ambayo
yametengwa huko vijijini msimu ujao wa mavuno ya mazao ya chakula.
Agizo
hilo amelitoa leo katika ziara yake ya siku tatu ya kutembelea na kuona
maendeleo ya sekta mbalimbali mkoani Ruvuma, na kuhakikisha kwamba
anatekeleza agizo la Rais John Magufuli linalosema hakuna Mtanzania
atakayekufa njaa.
Alieleza kwamba, wafanyabiashara ambao wamekuwa
wakipatiwa magunia na NFRA kwa ajili ya kununulia mahindi na wakulima
wanapojaribu kutafuta namna ya kuyapata magunia hayo, imekuwa ni tatizo
kwao kuyapata kwa urahisi.
Vilevile Waziri Mkuu, Majaliwa
alionesha kusikitishwa na vitendo hivyo vinavyofanywa na wafanyabiashara
wajanja, ambao wamekuwa wakipita vijijini kuwarubuni wakulima na
kununua mahindi kwa bei ndogo ambayo hailingani na uzalishaji wa zao
hilo.
Alisema kuwa kumekuwa na mianya ya rushwa inayofanywa na
wafanyabiashara hao kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa Wakala
huyo, kwa lengo la kujinufaisha watu wachache huku mkulima wa kawaida
akiendelea kuteseka na mazao yake shambani, jambo ambalo hivi sasa
limekuwa ni kero kubwa hasa katika maeneo ambayo mazao ya chakula
huzalishwa kwa wingi.
“Magunia yanayonunuliwa na serikali kwa
ajili ya kuhifadhia zao hili, ninazo taarifa za kutosha kwamba
hayamfikii mkulima kule kijijini, badala yake yanaishia kwa watu
wachache”, alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Vilevile alieleza kuwa
serikali inawajibu wa kuhifadhi chakula katika mazingira yanayokubalika
ili kisiweze kuharibiwa na wadudu waharibifu wa mazao, hivyo ameitaka
Wakala wa hifadhi ya taifa ya chakula kanda ya Songea kuhakikisha kwamba
mahindi yaliyohifadhiwa chini ya ardhi yanatafutiwa sehemu nyingine ya
kuhifadhia ili yasiharibike.
Alifafanua kuwa uhifadhi wa nje wa
zao hilo, usalama wake ni mdogo kwa asilimia 75 tu na kwamba mlundikano
huo wa magunia yaliyosheheni mahindi katika hifadhi hiyo ya chakula
unasababishwa na hifadhi kuwa na upungufu mkubwa wa maghala.
Pamoja
na mambo mengine, Waziri Mkuu Majaliwa alihoji juu ya msongamano wa
magari aina ya malori yaliyopo kando kando ya barabara ya kutoka Songea
kwenda Mbinga, huku akieleza kuwa hali hiyo imekuwa ikileta malalamiko
mengi kutoka kwa wasafirishaji kuwa magari yanayoingia NFRA kupakia
mahindi, huwapatia watu wanaojulikana kwanza, ndipo huruhusu wengine
kitendo ambacho kinaonyesha kuwa kuna upendeleo.
“Utaratibu
unaotumika kuingiza malori hapa kwenu una malalamiko mengi, taarifa
nilizonazo huingiza kwanza mtu anayejulikana, jambo hili likiendelea
linaweza kuleta mtafaruku au matatizo yasiyokuwa ya lazima, nahitaji
tatizo hili liwe mwisho na zingatieni haki na kupanga utaratibu mzuri”,
alisisitiza.
Awali Mbunge wa Jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma,
Leonidas Gama alisema kuwa tatizo la soko la mahindi katika mkoa huo ni
kubwa hivyo ameiomba serikali ya awamu ya tano, iangalie namna ya
kutafuta masoko ili wakulima wadogo waweze kupata fursa ya kuuza mazao
yao.
Gama alisisitiza kuwa ni vyema serikali irejeshe utaratibu
wa awali, wa NFRA kununua mahindi vijijini kwa wakulima na kuachana na
mfumo wa kuwatumia mawakala ambao hupita huko na kumkandamiza mkulima,
kwa kununua mazao yao kwa bei ndogo.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Chapisha Maoni