RPC RUVUMA MIHAYO MSIKHELA
NA GIDEON MWAKANOSYA, MBINGA.
MFANYABIASHARA mmoja ambaye
anajulikana kwa jina la Elias Mwalewela (46) anayeishi mtaa wa Manzese
Mbinga mjini mkoani Ruvuma amekamatwa akitorosha kahawa ya maganda
isiyokobolewa kiwandani kwenda Jijini Mbeya kwa njia ya magendo bila
kufuata taratibu na sheria husika.
Aidha imeelezwa kuwa wakati
zao hilo analitorosha, alikuwa akitokea wilayani Mbinga mkoani humo kwa
lengo la kuipeleka huko, huku akijua fika kahawa ya maganda hairuhusiwi
kusafirishwa kutoka wilaya moja kwenda nyingine.
Mkurugenzi
mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Venance Mwamengo alisema
kuwa baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema juu ya utoroshaji
huo, alichukua jukumu la kufuatilia suala hilo ndipo baadaye
alifanikiwa kumkamata katika kijiji cha Liganga wilaya ya Songea
vijijini mkoani hapa kwa kushirikiana na askari aliokuwa nao.
Alifafanua
kuwa alimkamata Disemba 30 mwaka jana, majira ya saa tano usiku akiwa
na gari aina ya Fuso lenye namba za usajili T 818 ADH ambalo lilikuwa
likiendeshwa na Geati Mwajungwa mkazi wa Lujewa Mbarali mkoani Mbeya.
“Huyu
mfanyabiashara na dereva wake, baada ya kuwakamata niliwafikisha kituo
kikuu cha Polisi wilaya ya Mbinga na gari lenye mzigo wa kahawa tani nne
ambalo linashikiliwa hapo kituoni, hivi sasa wanaendelea kuhojiwa na
taratibu zingine zitafuata ikiwemo kufikishwa Mahakamani au wanapaswa
kulipa faini ya shilingi milioni 20”, alisema Mwamengo.
Mwamengo
aliongeza kuwa watoroshaji hao walipofika mpakani mwa wilaya yake ambako
kuna geti la ukaguzi wa mazao, walitorosha gari hilo likiwa na kahawa
hiyo ndipo jitihada zilifanyika za kuwasaka na kufanikiwa kuwakamata
katika kijiji hicho cha Liganga.
Alieleza kuwa wakati
anawakamata, aliwakuta wakiwa na kibali cha usafirishaji kahawa safi
(Clean Coffee) ambacho ni cha kampuni ya Tutunze Kahawa Limited, iliyopo
wilayani humo ambayo inajishughulisha pia na ununuzi wa zao hilo.
Vilevile
aliongeza kuwa kwa mujibu wa taratibu husika, kibali hicho kinaruhusu
kusafirishia kahawa iliyo safi tu, ambayo imekwisha kobolewa kiwandani
na sio ya maganda kama walivyofanya watu hao.
Kufuatia tukio hilo
Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga naye alithibitisha juu ya tukio
hilo na kueleza kuwa mfanyabiashara huyo na dereva wa gari hilo
wanahojiwa na Jeshi la Polisi wilayani humo, ili waweze kutolea maelezo
ya kina juu ya kitendo hicho walichokifanya.
“Ni kweli taarifa
nilizonazo wamekamatwa wakisafirisha kahawa ya maganda (Mbuni) na wapo
Polisi wanahojiwa, wakimaliza kuhojiwa nitakuwa na taarifa kamili na
kulitolea ufafanuzi mzuri jambo hili hapo baadaye”, alisema Ngaga.
Hata
hivyo Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alipoulizwa kwa
njia ya simu juu ya tukio hilo alisema hataweza kutoa ufafanuzi wowote
kuhusiana na jambo hilo, akidai kwamba ofisi yake bado halijamfikia.
MWISHO.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Chapisha Maoni