0
Na Gideon Mwakanosya-Songea

MFUKO  wa Pension wa jamii( PPF) kama ilivyo moja ya majukumu ya mfuko huo umetoa elimu kwa wananchi wenye ulemavu wa kuto kusikia( Viziwi) 50 ambao wamepata elimu kuhusu hifadhi ya jamii na umuhimu wa kujiwekea akiba ya baadaye.

Hayo yalisemwa na meneja wa kanda ya kusini wa mfuko huo wa PPF  Kwame Temu wakati alipokuwa akitoa elimu jinsi namna ya kuweka akiba kwenye mfuko huo wa pension  wakati Mwananchi akiwa kwenye shughuli zake mbalimbali za kila siku zikiwemo za ujasiliamali .

Alieleza kuwa wote  Scheme ni mfumo maalum wa kuchangia unaohusisha sekta isiyo rasmi pamoja na ule mfumo wa ziada uliopo kwenye mfumo wa sekta iliyo rasmi hivyo lengo la mfumo huo wa wote scheme ni kukidhi mahitaji na kutambua mchango na ushiriki wa sekta isiyo rasmi kwenye uchumi na pia kutoa fursa mbalimbali kwa wajasiliamali pamoja na waendesha bodaboda.

Alieleza zaidi kuwa mfuko huo wa PPF ulikuwa umeandaa semina kwa ajili ya kuwapa elimu walemavu wasiosikia( viziwi) ambao wengi wao wapo katika mfumo usio rasmi kwa kuwapa elimu jinsi ya kujiunga na kulindwa na mfuko wa jamii pamoja na kufaidika na mafao mbalimbali kupitia mfuko huo.

Temu alitaja mafao yanayotolewa na PPF kuwa ni Afya kwa ajili ya kujali afya ya mwanachama wa PPF, Fao la uzeeni, Mkopo wa Elimu na mkopo wenye lengo la kutimiza ndoto ya mwanachama ambapo washiriki baada ya kuelewa umuhimu wa mafao hayo walijiunga na mfuko huo na kwamba semina hiyo ilikuwa na mafanikio makubwa.

Kwa upande wake Katibu mkuu mtendaji wa Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAMAVITA) Kelvin Nyema akichangia mada kwenye semina hiyo aliwaomba wabunge wa majimbo ya Peramiho, Madaba na Songea Mjini mkoani Ruvuma waone umuhimu wa kuwasidia walemavu viziwi  kuchangia angalau kwa kipindi cha miezi 6 kwa kila mmoja kama walivyoahidi kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana.

Nyema alieleza kuwa jinsi ya kuchangia kwa kiwango cha chini kuchangia kwa mwezi ni shilingi elfu ishirini(20,000/) ambacho kinawezwa  kulipwa aidha moja kwa moja kwenye akounti ya mfuko wa Pension wa PPF au kwa njia ya simu za mikononi za makampuni ya Vodacom (M-Pesa), kampuni ya AIR TEL (AIR TEL MONEY) na Kampuni ya TIGO( TIGO PESA) hivyo wabunge bado wanaombwa kuwasaidia walemavu viziwi ambao wamekuwa wakijishughulisha shughuli mbalimbali za ujasiliamali badala ya kupita mitaani kuomba .

MWISHO  

Chapisha Maoni

 
Top