0
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Zuber Mwombeji
 
NA STEPHANO MANGO,SONGEA
BAADHI ya wafanyabiashara wanaojishughulisha na uuzaji wa ng’ombe katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wamewalalamikia baadhi ya askari polisi waliokuwa doria kwa tuhuma za kumshushia kipigo na kumsababishia kifo chake Massanja Aliyo(38)aliyekuwa mlinzi kwenye eneo la machinjio ya ng’ombe katikati ya Manispaa ya Songea.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa masharti ya kutotajwa majina baadhi ya wafanyabiashara hao walieleza kuwa mei 8 mwaka huu majira kati ya saa 7 na saa 8 usiku kwenye eneo la machinjio ya ng’ombe Massanja inadaiwa kuwa alivamiwa na watu watatu ambao inadaiwa walikuwa wamevaa makoti marefu ya polisi.

Walifafanua Zaidi kuwa watu hao walimzingira na kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake kisha Massanja alijikuta akiwa mahututi na baadaye alifika mlinzi mwenzake ambaye hawakumtaja jina

Walisema kuwa baadaye watu hao watatu wasiofahamika wanaodhaniwa kuwa ni askari polisi ambao inadaiwa kuwa walivalia makoti,mizura na mabuti walikimbia na kutokomea kusikojulikana na baada ya muda mfupi askari polisi wakiwa kwenye gari walifika kwenye eneo la tukio na kuukuta umati wa watu waliofika kushuhudia baada ya kusikia kelele na baadaye kumchukua na kumkimbiza katika hospitali ya serikali ya mkoa ambako madaktari walithibitisha kuwa alikuwa amekwisha kufa.

Wameiomba serikali kupitia wizara ya mambo ya ndani kuona umuhimu wa kufanya uchunguzi yakinifu kufuatia kutokea kwa tukio hilo ambalo limegubikwa na utata mkubwa ambao umeleta hofu kwa wananchi kwa kutokuwa na Imani na askari polisi.

Kwa upande wake kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Zuber Mwombeji alipohojiwa na waandishi wa habari jana mchana ofisini kwake kuhusiana na tukio hilo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo alilitaja kuwa lilitokea mei 8 mwaka huu majira kati ya saa 7 na saa 8 usiku huko katika eneo la machinjio ya msamala ambako Massanja Aliyo mwenye asili ya kabila la kimasai alifariki dunia baada ya kupigwa na watu wasiofahamika.

Kamanda Mwombeji alisema kuwa Massanja kabla ya kukutwa na mauti alikuwa ni mfanyakazi wa Stamili Jeremia  katika machinjio ya Msamala ya kupokea ng’ombe toka Mbarari mkoani Mbeya na kuwalisha wakati wakisubiri kuchinjwa.

Mwombeji alisema kuwa katika uchunguzi wa awali wa polisi haukuona jeraha lolote kwenye mwili wa Massanja hata hivyo polisi inaendelea kufanya uchunguzi wa kina kubain ukweli juu ya watu waliohusika iwe raia au askari polisi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi na si vinginevyo.
MWISHO

Chapisha Maoni

 
Top