WAFANYABIASHARA RUVUMA WATAKIWA KUTUMBUANA WENYEWE
NA STEPHANO MANGO,SONGEA
WAFANYABIASHARA Mkoani Ruvuma wametakiwa kuwafichua wafanyabiashara wenzao wenye tabia ya kukwepa kulipa kodi ya serikali ikiwemo ya mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) ambao wanaisababishia serikali hasara na badara yake waone umuhimu wa kuwa waaminifu kwenye biashara zao na kulipa kodi ipasavyo na si vinginevyo.
Hayo yamesemwa jana na Katibu wa jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania (JWT) mkoani Ruvuma Wilson Nziku wakati alipokuwa akitoa taarifa ya mkutano mkuu wa jumuhiya hiyo uliofanyika jijini Dar es salaam kwa wafanya biashara walio hudhuria kwenye mkutano maalumu ulioitishwa na jumuhiya hiyo mjini songea.
Nziku maarufu kwa jina la Kipara alisema kuwa wafanyabiashara ambao si waaminifu wenye tabia mbaya ya kuto kulipa kodi hawafai hata kidogo kwani ndio wanaowachafulia wafanyabiashara wengine wenye tabia nzuri ambao wamekuwa wakilipa kodi kwa uwakika na sio kwa kusuasua .
Aliwaonya baadhi ya watumishi wa serikali wasio waaminifu ambao wamepewa dhamana ya kusimamia mamlaka ya mapato ambao inaonekana wanafanya kazi kwa malengo ya kujinufaisha badala ya kuinufaisha serikali ambayo imekuwa ikiwahudumia watanzania kwa kutoa elimu bure kwa wanafunzi wanaosoma
shule za msingi na Sekondari pamoja huduma ya afya kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano(5) na wazee.
Alisema kuwa kila mfanyabiashara ahakikishe anajikita zaidi katika kuboresha biashara anazozifanya kila siku na waacha tabia ya kufanya biashara kwa mazoea kwa kutumia njia za mikato ambazo zinaweza kudhoofisha biashara anazozifanya.
Naye mwenyekiti wa jumuhiya ya wafanyabiashara Tanzania (JWT) mkoani Ruvuma Isaya Mbilinyi alisema kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli imeonyesha wazi kuwa inahitaji wafanyabiashara waaminifu ambao ni walipa kodi ya serikali wazuri hivyo wafanyabiashara wote mkoa Ruvuma ni vyema wakaona umuhimu wa kuuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli.
Mbilinyi alisema kuwa kitendo cha Rais Dr. Magufuli cha kuwatumbua majipu viongozi wa serikali wasiokuwa waaminifu kimewafurahisha watanzania wengi na kimeijengea imani serikali yao hivyo ni vyema sasa kila mtanzania akaona umuhimu wa kujenga nidhamu katika sehemu za kazi anazozifanya pia na wafanyabiashara ni vyema wakawa na nidhamu kwa watumishi wa mamlaka ya mapato pale wanapokwenda kuwapa ushauri yakinufu namna ya kulipa kodi na si
vinginevyo.
MWISHO
Chapisha Maoni