0
   Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Ruvuma Zuberi Mwombeji
NA STEPHANO MANGO,SONGEA

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linamsaka dereva wa Daladala inayofanya kazi ya kusafirisha abiria la kutoka Songea kwenda Peramiho ambaye jina lake alikuweza kufahamika mara moja kwa tuhuma za kuigonga pikipiki kisha kuacha njia na kumgonga mtembea kwa miguu na kuwasababishia vifo mwendesha pikipiki na mtembea kwa miguu papo hapo.

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Ruvuma Zuberi Mwombeji alimtaja mwendesha boda boda aliyefariki dunia kuwa ni Frenk Mahundi (18) mkazi wa Lizaboni Manispaa ya Songea na mtembea kwa miguu ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja anayekadiliwa kuwa na umri kati ya 20 na 25 wa jinsia ya kiume.

Alisema kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio Juni 20 mwaka huu majira ya saa 11 jioni huko katika eneo la mtaa wa mkomi kwenye barabara ya kutoka Songea kwenda Mbinga gari lenye namba za usajiri T811AHG aina ya nissan Caravan ambayo ilikuwa ikiendeshwa na dereva ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja ilimgonga mwendesha boda boda Mahundi na kumsababishia kifo papo hapo.

Alifafanuwa kuwa baadae gari hilo liliacha barabara kisha lilimgonga mtembea kwa miguu ambaye jina lake halikuweza kufahamika wa jinsia ya kiume na kumsababishia kifo papo hapo na baada ya tukio hilo dereva wa gari hilo ambalo lilikuwa limesheheni abiria alikimbia na kutokomea kusiko julikana.

Alieleza zaidi kuwa mwili wa Mahundi ulichukuliwa na ndugu zake ambao walikuja kuutambua na mwili wa mtembea kwa miguu mpaka sasa bado umehifaadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia mahiti kwenye hospitali ya serikali ya Mkoa wa Songea(HOMSO) na kwamba wananchi wameshauriwa kwenda kuutambua mwili wa marehemu .

Kamanda Mwombeji alisema kuwa jeshi la polisi linaendelea kumsaka dereva wa gari hilo na kwamba chanzo cha ajari hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa daladala ambao ulimfanya ashindwe kumudu usukani.

MWISHO. 

Chapisha Maoni

 
Top