NA STEPHANO MANGO,SONGEA
Utafiti umebaini kuwa matumizi ya dawa za kulevya
hasa kwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 45 bado ni tatizo kubwa
katika Halmashauri ya manispaa ya Songea.
Ofisa
habari wa manispaa ya Songea Albano Midelo amesema takwimu zilizopo zinaonesha
kuwa katika kipindi cha mwaka 2015 Manispaa hiyo ilikuwa na Waathirika wa
madawa ya kulevya 145 kati ya hao Wanaume ni 138 na Wanawake ni saba.
Amesema
katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Mei, 2016 Manispaa ya Songea
ina jumla ya waathirika wa Madawa ya
kulevya 97 kati yao Wanawake wawili na Wanaume 95 ambapo waathirika wote wakiwa na
umri kati ya miaka 15 hadi 45.
Kutokana na hali hiyo ametoa rai kwa wadau
mbalimbali kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya madawa ya kulevya ili kujenga jamii na maisha na utu wa mtu bila matumizi
ya dawa za Kulevya
ambazo ni tatizo sio kwa manispaa ya
Songea bali pia vijana wengi katika nchi nzima.
Mganga
mkuu wa manispaa ya Songea Dr.Simon Chacha amesisitiza kuwa kuongezeka kwa Tatizo
la matumizi ya dawa za kulevya katika Manispaa ya Songea linadhihirishwa na
kuwepo kwa waathirika wa dawa za kulevya mitaani na wale wanaofika Hospitalini.
“Athari
za matumizi ya dawa za kulevya katika Jamii ni pamoja na kupungua kwa nguvu kazi, uporaji mali,
ubakaji na ongezeko la maambukizi ya Ukimwi hivyo kupunguza nguvukazi ya taifa
kwa kuwa na vijana wengi wagonjwa na wengine wanafariki Dunia’’,alisema.
Hata
hivyo alisema Kutokana na Athari za dawa za kulevya katika Manispaa ya Songea ametoa wito kwa vijana na
kwa Wananchi wote kutojihusisha kwa namna yeyote kutumia dawa haramu za
kulevya.Pia anawashauri wale wote walioathirika na dawa za kulevya kwenda
kwenye vituo vya Afya kupata tiba na ushauri nasaha.
Mkuu wa wilaya ya Songea Benson
Mpesya katika risala ya utii kwa Rais wakati wa mbio za mwenge wa uhuru Juni 8
mwaka huu katika manispaa ya Songea alibainisha kuwa katika kukabiliana na dawa
za kulevya elimu sahihi inatolewa kwa vijana ili wajiepushe na matumizi ya dawa
za kulevya na kuwafichua wote wanauza,kulima na kutumia dawa hizo haramu.
Aliongeza kuwa kupitia mfumo wa
polisi jamii wananchi wengi wamejitokeza kuwafichua wote wanaojishughulisha na
biashara hiyo haramu ambapo msako wa kuwabaini unafanyika katika mitaa yote
mjini Songea ili kukomesha biashara hiyo haramu.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru
mwaka 2016 George Mbijima akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya
Songea waliteketeza dawa za kulevya kwenye viwanja vya shule ya msingi Mloweka
mjini Songea zilizokamatwa na polisi katika manispaa ya Songea mwaka huu.
Mwisho
Chapisha Maoni