Halmashauri ya
manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imefikia asilimia 98 katika utengenezaji wa
madawati hadi kufikia Juni 20 mwaka huu.
Ofisa habari wa
manispaa hiyo Albano Midelo amesema manispaa hiyo katika kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kumaliza kero ya
madawati inaendelea kutengeneza na kukamilisha madawati 5,130 yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 333.45 ambayo
yanahitajika katika manispaa ya Songea.
Hata hivyo
amesema hadi kufikia mwezi Juni Madawati
yote yaliyokwisha tengenezwa ni zaidi ya 5000 kati ya madawati 5130 ambayo sawa
na zaidi ya asilimia 98 ya mahitaji ya
madawati yote katika manispaa hiyo.
Kaimu afisa elimu wa manispaa ya Songea Sunday Wahyungi amesema Mradi wa madawati katika manispaa hiyo ulianza tangu mwezi wa Desemba
mwaka 2015 ikiwa ni utekelezaji wa agizo
la Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania iliyowataka Wakuu wa Mkoa,Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi
kuhakikisha kuwa hakuna wanafunzi wanaokaa chini hadi kufikia Juni 30 mwaka huu.
Wahyungi amesisitiza kuwa kabla
ya Juni 30 hakuna mwanafunzi ambaye atakaa chini katika shule za msingi za
manispaa hiyo kwa kuwa madawati yote yaliopangwa kukamilisha mradi wa madawati
yatakuwa yametengezwa hivyo uhaba wa madawati katika manispaa ya Songea kubakia
kuwa historia.
Kwa upande wake
mkuu wa wilaya ya Songea Benson Mpesya amesisitiza kuwa hadi kufikia Juni 25
mwaka huu miradi yote ya madawati katika wilaya hiyo itakuwa imekamilika hivyo
kumaliza kabisa tatizo la baadhi ya wanafunzi katika shule kukaa chini kutokana
na upungufu wa madawati.
Mpesya ambaye
pia ni kaimu mkuu wa mkoa wa Ruvuma amesema wilaya ya Songea imefikia hatua
nzuri ya utengenezaji wa madawati ambapo hati kufikia Juni 22 miradi yote ya
madawati itakuwa imekamilika katika manispaa ya Songea.
Amezitaja
wilaya nyingine za mkoa wa Ruvuma ambazo utengenezaji wa madawati umefikia
zaidi ya asilimia 80 kuwa pamoja na
Namtumbo,Mbinga,Nyasa na Tunduru na kwamba taarifa alizonazo ni kwamba hadi
kufikia Juni 28 miradi ya madawati katika wilaya zote itakuwa imekamilika.
Amewaagiza
watendaji katika ngazi zote katika mkoa wa Ruvuma kusimamia zoezi la
utengenezaji wa madawati yaliobakia
kabla ya Juni 30 ili kuhakikisha
kuwa kuanzia mwezi Julai mwaka huu tatizo la madawati katika shule za mkoa wa
Ruvuma ibakie kuwa historia.
Mwisho
Chapisha Maoni