NA STEPHANO MANGO,SONGEA
MIAKA mitano ijayo manispaa
ya Songea mkoani Ruvuma inatarajiwa kuwa kituo kikubwa cha utalii katika
ukanda wa kusini.
Ofisa habari wa manispaa hiyo Albano Midelo alisema mbunge
wa Songea mjini Leonidas Gama akizungumza na wakuu wa idara na vitengo wa
manispaa ya Songea kwenye ukumbi wa manispaa hiyo alisema hadi kufikia mwezi
Septemba mwaka huu barabara ya kutoka Mtwara hadi Mbinga inatarajiwa kuwa lami.
Gama amesema mara baada ya barabara hiyo kukamilika fursa za
uwekezaji hasa katika sekta ya utalii zilizopo manispaa ya Songea zitavutia
wawekezaji wengi wa ndani na nje ya nchi na kufika kuwekeza hali ambayo
itaongeza mapato na ajira kwa wakazi wa manispaa hiyo.
“Mtwara kuna
wawekezaji ambao wapo kutokana na
kugundulika gesi,wawekezaji hawapendi joto hivyo watapenda kutembelea maeneo
yenye hali nzuri ya hewa kama Songea ili kutalii,hivyo fursa za utalii zilizopo
manispaa ya Songea zitaongeza uwekezaji’’, alisema Gama.
Gama amesema mazingira ya Songea kutokana na hali ya hewa na
vivutio adimu vya utalii itakuwa ni kituo kikuu cha utalii hivyo kufungua
milango ya utalii kusini kuanzia Mtwara hadi
mwambao mwa ziwa Nyasa.
Kutokana na hali hiyo amewataka watalaam wa manispaa ya
Songea kuanza kuboresha vivutio ambavyo vitawavutia wawekezaji hasa ujenzi wa
hoteli bora,nyumba za kulala wageni,miundombinu bora ya umeme,kuboresha kiwanja
wa ndege cha Songea pamoja na kuvitangaza vivutio vyote vya utalii vilivyopo.
“Ingieni kwenye mtandao,tafuteni fursa za uwekezaji zipo.Kwa
mfano wajerumani ni wawekezaji wazuri
ambao wanaangalia fursa na kukutafutia wawekezaji moja kwa moja,hivyo Songea
tuwatumia hao ili kuendeleza sekta ya utalii ambayo inachangia pato la Taifa’’,alisisitiza.
Mchumi wa manispaa ya Songea Raphael Kimary anavitaja
vivutio adimu vya utalii vilivyopo katika manispaa hiyo kuwa ni makumbusho ya Taifa ya Majimaji,hifadhi ya
asili ya Luhira na vivutio vingine vya
kishujaa na kiutamaduni.
“Manispaa ya Songea ni chanzo cha bonde la Mto Ruvuma ambao unatiririsha maji
katika baharí ya Hindi na Mto Ruhila ambao hutiririsha maji katika ziwa
Nyasa.Mtiririko wa maji ya mito hutegemea majira ya mwaka, huwa mengi wakati wa
mvua’’,alisema Kimary.
Hata hivyo
amesema Sehemu kubwa ya Manispaa ya Songea
ina umbile la tambarare, mwinuko wa Milima Matogoro na Unangwa na kwamba
Manispaa ipo katika mwinuko wa nchi kutoka usawa wa baharí kati ya mita 980 na
1500.
Halmashauri
ya Manispaa ya Songea ni miongoni mwa Halmashauri tatu zilizopo katika wilaya
ya Songea ikiwa na kata 21 na mitaa 95.Halmashauri nyingine zinazounda wilaya
hiyo ni Halmashauri ya wilaya ya Songea na Madaba.
Mwisho
Chapisha Maoni