MBUNGE ALIYEPIGWA CHINI JIMBO LA MBINGA GAUDENCE KAYOMBO AKIHUZUNIKA
NA STEPHANO MANGO, MBINGA
KUFUATIA
vuguvugu la kisiasa ambalo limeendelea kushika kasi na kutishia hali ya
amani katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Mbinga mkoa wa
Ruvuma, kutokana na wananchi kuutaka uongozi husika wa chama hicho
wilayani humo utangaze matokeo ya nafasi ya ubunge uchaguzi kura za
maoni, hatimaye matokeo hayo yalitangazwa kwa jimbo la Mbinga vijijini
majira ya saa 5:45 usiku.
Kabla
ya kutangazwa kwa matokeo hayo kwa jimbo hilo, kulikuwa na mvutano
mkali ambao ulidumu kwa masaa 12, kutokana na kati ya wagombea nane
waliokuwa katika kinyang’anyiro hicho, mgombea Gaudence Kayombo kudaiwa
kufanya mchezo mchafu wa kutaka kuchakachua matokeo kwa kata ya Ruanda
na Kihangimahuka, ili yaweze kumpatia ushindi baada ya kuona hali ya
upepo wa ushindi kwa upande wake inamwendea vibaya.
Aidha
kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi wilayani humo lililazimika askari
wake kuweka ulinzi mkali katika eneo la ofisi hizo za CCM, kutokana na
baadhi ya wanachama kuleta vurugu huku wengine wakirusha mawe.
Baadhi
ya wanachama wa chama hicho waliendelea kuandamana maeneo mbalimbali ya
mji wa Mbinga, wakitishia kutoondoka katika maeneo ya ofisi za CCM na
kuonekana kuranda randa huku wakiimba nyimbo mbalimbali na kutamka
maneno…………….“hapa mpaka kieleweke, tunachotaka ni matokeo na sio
vinginevyo”.
Sinto
fahamu iliendelea kutawala katika eneo la ofisi za CCM wilaya ya Mbinga
ambapo wanachama wa chama hicho walionekana kuendelea kujawa jazba na
kuutaka uongozi husika utangaze matokeo ya nafasi hiyo ya ubunge,
kutokana kucheleweshwa kutangazwa.
“Tunataka
matokeo, tunataka matokeo, tunataka matokeo hapa mkitaka amani
tuleeteeni matokeo vinginevyo tunarudisha kadi za CCM hatukitaki chama
tunataka haki itendeke kwa mshindi aliyeshinda”, hayo ni maneno ambayo
yalikuwa yakitawala katika eneo la ofisi kuu za chama hicho wilayani
humo ambayo yalikuwa yakitamkwa na wanachama wa chama hicho.
Kadhalika
licha ya Katibu wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma, Verena Shumbusho
kujitokeza mbele ya hadhira hiyo ambayo ilionekana kudai matokeo hayo
katika viwanja vya chama hicho, bado wanachama walionekana kujawa jazba
wakitamka maneno ya kutaka matokeo yatangazwe na wengine wakiendelea
kutamka hawawezi kuondoka mpaka kieleweke.
“Ndugu
zangu tulizeni jazba, lazima tufuate utaratibu wa chama, hatuwezi
kuendesha chama kwa mashinikizo”, alisikika akisema Shumbusho mbele ya
umati huo uliokuwa kwenye viwanja vya CCM mjini hapa.
Baadhi
ya wanachama waliendelea wakisema, wanamashaka na viongozi wa wilaya
hiyo wakiwemo chama na serikali, huenda wanapanga mpango wa kutaka
kuyachakachua matokeo ili atangazwe mgombea ambaye sio chaguo sahihi la
wananchi.
Waandishi
wa habari ambao walikuwa wakishuhudia juu ya sakata hilo na kumtaka
Katibu wa wilaya hiyo, Zainabu Chinowa azungumzie juu ya hali hiyo
alisema kuwa mpaka sasa wanashindwa kutangaza matokeo kutokana na jimbo
hilo la Mbinga vijijini katika kata ya Ruanda na Kihangimahuka, kuwepo
kwa utata juu ya matokeo ya nafasi ya ubunge.
“Ndugu
zangu waandishi wa habari chama kimetuma magari huko Kihangimahuka na
Ruanda kufuatilia juu ya suala hili, kwa sababu matokeo yanaleta utata
kidogo, hivyo yakiletwa na chama kujiridhisha juu ya jambo hili
tutayatangaza muda wowote hata kama itakuwa ni usiku nawaomba wananchi
waache jazba wakati tunaendelea na mchakato huu”, alisema Chinowa.
Kadhalika
baada ya kukamilika kwa taratibu husika za chama ndipo matokeo kwa
nafasi ya ubunge wa jimbo la Mbinga vijijini yalitangazwa Agosti 3 mwaka
huu majira ya saa 5:45 usiku ambapo, Martin Msuha aliweza kuchukua
nafasi ya ushindi katika jimbo hilo kwa kupata kura 13,354 na
kuwagaragaza chini wagombea wenzake saba, waliokuwepo kwenye
kinyang’anyiro hicho.
Wagombea
wengine waliokuwa wakiwania nafasi hiyo na kura walizopata katika
mabano kuwa ni; Humprey Kisika (545), Dokta Silverius Komba (1,289),
Edesius Kinunda (2,355), Deodatus Mapunda (2,532), Benaya Kapinga
(3,941), Deodatus Ndunguru (7,060) na Gaudence Kayombo aliyepata kura
12,068.
Pamoja
na mambo mengine, wilaya ya Mbinga ambayo ina majimbo mawili ya
uchaguzi Mbinga mjini na vijijini ambapo kwa upande wa jimbo hilo la
mjini matokeo yake kwa nafasi ya ubunge yanatarajiwa kutangazwa leo
majira ya jioni, baada ya kumalizika kwa uchaguzi mdogo ambao unaendelea
katika kata ya Kikolo na Uzena zilizopo wilayani humo.
MWISHO.

Chapisha Maoni