AFISA ELIMU MKOA WA RUVUMA MAYASA HASHIMU
NA STEPHANO MANGO,SONGEA
KITENDO cha kusitisha zoezi la Wazazi
kuchangia chakula, kwa shule za sekondari za kutwa za serikali zilizopo
katika Manispaa ya Songea mkoani humo baadhi ya Wakuu wa shule hizo
wamesema kwamba, ni ukiukwaji wa maagizo yaliyotolewa na serikali
kupitia mwongozo wake uliosambazwa katika mikoa yote hapa nchini.
Aidha
kufuatia hali hiyo shule hizo ambazo sasa zimefunguliwa na kuanza
muhula wa masomo Januari 11 mwaka huu, nimeshuhudia watoto wakikosa
chakula shuleni huku wakilazimika kuhudhuria vipindi vya masomo darasani
bila kula chakula, kuanzia majira ya asubuhi hadi saa 10:00 jioni
wanaporejea majumbani kwao.
Ukiukwaji huo wa agizo la serikali,
wanasema kuwa unathibitisha kufuatia mwongozo uliotolewa na Ofisi ya
Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Novemba 23
mwaka jana (nakala tunayo) wenye kumbu kumbu namba DC. 297/507/01/146
katika kipengele cha 4 ukielekeza kwamba majukumu ya mzazi ni pamoja na
kuhakikisha kwamba huduma ya chakula kwa wanafunzi wa kutwa anachangia,
yakiwemo na mahitaji mengine ya kibinadamu kama vile sare za shule na
michezo, matibabu, vifaa vya kujifunzia ikiwemo daftari na kalamu.
Vilevile
mzazi akiwa sehemu ya mwananchi na jamii inayozunguka shule husika,
atashiriki kikamilifu katika kazi ya ujenzi wa miundombinu ya shule kwa
kuchangia nguvu zao kadri itakavyoamriwa na mkutano husika wa kijiji,
mtaa, kata au tarafa.
Uchunguzi wa mwandishi wetu umebaini
kwamba, sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 na ilani ya uchaguzi ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 hadi 2020 ibara ya 52 (a)
imebainisha kwamba serikali itatoa elimu bure kwa ngazi ya elimu awali,
msingi hadi kidato cha nne bila malipo ya ada na michango mingine ya
uendeshaji wa shule kuanzia mwaka wa masomo wa 2016, lakini haitamki
kwamba mzazi asichangie chakula cha mtoto wake shuleni kwa shule hizo za
kutwa.
Serikali kuu na mamlaka za serikali za mitaa zitaendelea
kugharimia uendeshaji wa shule, kwa kutoa ruzuku na fedha ya chakula kwa
shule maalumu za msingi na sekondari za bweni na sio zile za kutwa,
kugharimia pia taaluma, madawati na ukamilishaji ujenzi wa majengo ya
shule.
Pia walimu hao wa shule za sekondari za kutwa katika
Manispaa ya Songea nimezungumza nao kwa nyakati tofauti, wameeleza kuwa
usitishaji wa mchango wa chakula kutoka kwa wazazi ni agizo lilitolewa
na Ofisa elimu wa sekondari mkoani humo, Mayasa Hashim kwani wao
walikwisha andaa na kufuata utaratibu wa mzazi kuchangia chakula kadri
ya mwongozo huo uliotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, kuhusiana na shule hizo hapa nchini zinavyopaswa
kuchangia.
Walisema kuwa kufikia Disemba 21 mwaka jana, wakuu wa
shule za sekondari katika Manispaa hiyo wote waliitwa na kupewa mwongozo
huo uliotolewa na TAMISEMI huku wakisisitizwa kufuata yaliyomo ndani
yake.
“Baada ya kupewa tuliambiwa na kusisitizwa tufuate yaliyomo
katika mwongozo huu, wakuu wa shule wote tulifanya hivyo tunachotambua
michango na ada imefutwa lakini chakula kwa shule za kutwa mzazi lazima
achangie”, walisema.
Hata hivyo alipohojiwa na waandishi wa
habari ofisini kwake, Ofisa elimu wa shule za sekondari mkoa wa Ruvuma
Mayasa Hashim alikiri kusitisha kwa mchango wa chakula na michango
mingine kutoka kwa wazazi, huku akiongeza kuwa utaratibu mwingine
unaandaliwa na tayari wakuu wote wa shule za sekondari za kutwa katika
Manispaa hiyo, wamepewa maelekezo ya kufanya juu ya suala hilo.
MWISHO
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Chapisha Maoni